Home

▼

Tuesday, 3 December 2013

WABUNGE UKRAINE WANA IMANI NA SERIKALI YAO

Bunge la Ukraine limeepuka kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Rais Viktor Yanukovych. Pendekezo lililowasilishwa na upinzani la kutaka serikali ipigiwe kura ya kutokuwa na imani nayo limepata kura 186, dhidi ya 226, ambazo zingeliwezesha kupita. Kura hiyo iliitishwa kutokana na maandamano ya umma yaliyochochewa na uamuzi wa serikali na Rais Yanukovych kutosaini mkataba wa kihistoria na Umoja wa Ulaya, na badala yake kuimarisha uhusiano wa karibu na Urusi. Maelfu ya waandamanaji waliokusanyika nje ya jengo la bunge walipiga kelele wakitamka maneno kama vile 'Aibu' na 'Mapinduzi', baada ya kugundua matokeo ya kura hiyo. Chama tawala cha Rais Yanukovych cha Regions, ambacho kina wingi bungeni, kilisema hakitaliunga mkono pendekezo hilo. Hayo yanajiri wakati Waziri Mkuu, Mykola Azarov akiomba radhi kutokana na vitendo vya mabavu vilivyofanywa na polisi mwishoni mwa juma lililopita. Ukandamizaji huo ulilaaniwa vikali na mataifa ya Magharibi na kuzusha maandamano makubwa zaidi.

No comments:

Post a Comment